Tuesday, February 5, 2013

Na Hamida Khalid, Babati NYUMBA zipatazo 6 zimechomwa moto katika kijiji cha Manyara, kata ya Bagara, Wilaya ya Babati Mkoani Manyara na kuteketezwa kabisa samani zake za ndani pamoja na mifugo wakiwemo mbuzi 64 na kuku zaidi ya 30. Nyumba hizo ambazo zilichomwa moto na wananchi wanaosadikiwa kuwa ni wa kijiji cha jirani cha Bagara kinachopakana na kijiji hicho ni pamoja na nyumba ya Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Barikiely Amsi ambaye pia mifugo yake yote iliteketea. Akiongea na mwananchi katika eneo la tukio Bw. Amsi alieleza kwamba tukio hilo limetokea Februari 3 majira ya jioni ambapo baadhi ya watu wa maeneo hayo wakiwa katika shughuli zao za kujitafutia na yeye na familia yake wakiwa miongoni mwao. Alisema kuwa kilichomshitua kurudi nyumbani kwake alisikia watu wakipiga mayowe kuomba msaada ndipo walipokimbilia eneo hilo na kukuta nyumba sita zilizofuatana zikiwa zinateketea kwa moto. "Wanakijiji tulijitahidi kuzima moto huo tukafanikiwa lakini hakuna kitu hata kimoja tulichofanikiwa kuokoa, wenzangu wameunguliwa vitu vyote vya ndani na mimi pia pamoja na mbuzi 64 na kuku walikuwemo zaidi ya 30, kama mnavyoona hapo mbuzi wanavyomalizikia kuteketea" alisema Bw. Amsi. Aidha Mwenyekiti huyo aliwataja wenzake waliopatwa na mkasa huo kuwa ni pamoja na Bw. Emanuel Halaay, Bw. Shamba Emanuel, Bw. Tiay Nyerere, Bw. Badada Sule na Bw. Maasai Matte. Wakati tukio hilo loikitokea kulikuwepo na baadhi ya wanakijiji ambao walijitambulisha kuwa ni majirani waliopakana na nyumba ya mwenyekiti na kueleza jinsi walivyoona moto ukishika kwenye nyumba hizo na kusema kuwa waliona zikiwaka kwa pamoja. "Wakati moto unawaka nyumba ya nne kutokea hapa kwa mwenyekiti mimi nilikuwepo eneo lile nilipoona moto unawaka nikasogea karibu, nikagundua ni nyumba inaungua ndipo nikaanza kukimbia ili kuita wenzangu, wakati nakuja huku nikaona na nyumba zinazofuata nazo zinaungua ndipo nikapiga yowe kuomba msaada" alisema Bw. Banga Bura ambaye ni jirani wa Bw. Amsi. Kwa upande wake Mtendaji wa kijiji hicho Bi. Selina Emanuel alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwepo nyumbani kwake ambapo ni mbali kidogo na eneo la tukio hivyo alichelewa kufika na kukuta tayari nyumba zimekwishateketea. "Kwakweli mimi sina hata cha kuelezea kwakuwa sikuwepo eneo la tukio, nilipata taarifa kwa njia ya simu hivyo wakati najiandaa kuja polisi walishafika na tayari mtu mmoja ameshakamatwa yuko mikononi mwa polisi kuhusiana na tukio hilo" alifafanua Mtendaji huyo. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Manyara Bw. Akili Mpwapwa alisema kuwa watu wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo kupitia kwa wasiri wa polisi waliokuwepo katika eneo hilo. Kamanda Mpwapwa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Marco Alli (42) na Iddi Athumani (27) wote wkulima na wakazi wa kijiji cha Magara na kubainisha kwamba chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Manyara na kijiji cha Magara. Mwisho.